Klabu ya Yanga imetangaza rasmi kalenda ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2026, ambao mchakato huo utaanza Juni 25, 2026 na kuhitimishwa kwa upigaji kura Agosti 2, 2026.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Kamati ya Uchaguzi imeweka hatua mbalimbali zitakazowapa wanachama nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi watakaoiongoza klabu hiyo kwa kipindi kijacho.
“Leo tuna agenda moja tu ambayo ni uchaguzi wa Yanga Sc, kama mnakumbuka hivi karibuni tulizindua uchaguzi wa matawi. Baadhi ya matawi yamefanya na mengine yanaendelea kwa wale ambao hawajaleta majina ya viongozi tunasisitiza kufikia 7 Julai wawe wamemaliza” alisema Adv. Malangwe Mchungahela Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi
Mchakato huo utaanza kwa kutangazwa kwa uchaguzi na nafasi zinazogombewa huku fomu za kugombea zikitolewa kuanzia Juni 25 hadi Juni 29, 2026. Baada ya hapo kutafanyika kikao cha mchujo wa awali wa wagombea kabla ya orodha ya majina ya awali kutangazwa rasmi.
“Napenda kuchukua fursa hii kutangaza uchaguzi mkuu wa Yanga. Uchaguzi mkuu imepangwa kufanyika Agosti 2, 2026 ambapo wanachama wa Yanga SC watapiga kura kuwachagua viongozi wapya wa klabu hiyo na kuanzia kesho fomu zitatolewa hapa Yanga. Ibara ya 26 ya Yanga ndio inatoa sifa za wagombea. Fomu ya Rais na makamu wa Rais 200,000 na fomu kwa wajumbe ni 100,000.” aliongeza Mchungahela
Wagombea watapatiwa nafasi ya kuwasilisha pingamizi dhidi ya matokeo ya mchujo, ambapo Kamati ya Uchaguzi itafanya usaili na hatimaye kutangaza orodha ya wagombea waliokidhi vigezo vya kuendelea na mchakato huo.
Aidha, Kamati ya Uchaguzi imeweka nafasi kwa rufani kupitia Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kwa wale watakaokuwa hawajaridhishwa na maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya Yanga SC. Rufani hizo zitawasilishwa katikati ya mwezi Julai kabla ya kutolewa kwa maamuzi ya mwisho.