Aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga SC, Prince Dube, ametoa ujumbe wa hisia kali kuwaaga mashabiki wa klabu hiyo kufuatia kumalizika kwa safari yake ya misimu miwili akiwa Jangwani.
Dube, ambaye tayari amejiunga na Hardrock FC ya Zimbabwe, amesema Yanga haikuwa klabu ya soka pekee kwake bali imekuwa familia iliyompa nafasi ya kuaminiwa na kuonyesha uwezo wake wakati ambao wengi hawakuwa na imani naye.
"Wananchi, sijui hata nianzie wapi kwa sababu nashindwa kupata maneno sahihi ya kusema. Ninapozungumzia klabu hii, naona watu walioamini, walionipenda na kuona mwanga ndani yangu wakati hata sikustahili hilo. Ninaona watu waliosimama kando yangu wakati ulimwengu ulikuwa kinyume changu. Watu walipoona kushindwa, nyinyi mliona kitu maalum ndani yangu," amesema Dube.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Zimbabwe ameongeza kuwa kutokana na upendo alioupata kutoka kwa mashabiki wa Yanga, klabu hiyo itaendelea kuwa na nafasi ya kipekee moyoni mwake.
"Sioni tu hii kama klabu ya mpira wa miguu bali naiona kama familia, na kwa hilo mtakuwa na nafasi maalum moyoni mwangu kila wakati."
Katika ujumbe wake, Dube aliwashukuru viongozi wa Yanga akiwemo mfadhili wa klabu, GSM, Rais wa Yanga, Hersi Said, benchi la ufundi, wachezaji wenzake, wafanyakazi wa klabu pamoja na familia yake kwa mchango wao katika mafanikio aliyoyapata akiwa ndani ya kikosi hicho.
"Nataka kuchukua fursa hii kumshukuru Boss GSM, Rais wa Timu Bw. Hersi, wachezaji wenzangu, makocha wote walionipa fursa ya kuonyesha kipaji changu, bila kumsahau mke wangu mrembo na familia yangu kwa kuniunga mkono tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho."
Hata hivyo, alisema kundi ambalo litabaki kuwa la kipekee kwake ni mashabiki wa Yanga ambao walikuwa wakimpa nguvu kila alipokuwa uwanjani.
"Lakini muhimu zaidi ni mashabiki. Nyinyi kila wakati mmekuwa maalum kwangu kwa kunitia moyo katika kila siku niliyocheza. Asante kwa kuifanya safari hii kuwa ya kushangaza. Najinyenyekeza kwa kila kitu nilicho nacho na nasema Asante Wananchi, Asante sana."
Dube anaondoka Yanga baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa misimu miwili tangu alipojiunga akitokea Azam FC. Katika kipindi hicho alikuwa mmoja wa washambuliaji muhimu waliochangia mafanikio ya Wananchi, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku msimu uliomalizika akifunga mabao 10 na kuonyesha uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali kwenye safu ya ushambuliaji.