Kiungo mshambuliaji wa Azam Fc Iddi Suleiman 'Nado' amethibitisha kuwa mkataba wake na klabu hiyo umemalizika akigoma kuweka wazi kama ataendelea kusalia viunga vya Chamazi huku tetesi zinazomuhusisha na Yanga zikiendelea kupamba moto.
Chanzo cha uhakika ndani ya uongozi wa Yanga, kimethibitisha kuwa mabingwa hao wa ligi kuu wamefungua mazungumzo na wawakilishi wake ili kumsajili.
Yanga ilianza kumfuatilia Nado wiki kadhaa zilizopita baada ya kubaini mkataba wake unaelekea ukingoni huku akiwa hajasaini mkataba mpya.
Nado ni mchezaji anayeweza kuongeza makali kwenye eneo la washambuliaji wanaotokea pembeni (mawinga). Amekuwa katika kiwango bora msimu wa 2025/2026 akiwa miongoni mwa wachezaji muhimu ndani ya Azam FC.
Takwimu zake zinaonyesha mchango mkubwa akihusika kwenye mabao 13, akifunga mabao 8 na kutoa pasi 5 za mabao.
Uwezo wake wa kucheza pembeni, kupiga krosi maridhawa na kushambulia kwa kasi umeifanya Azam FC kunufaika naye katika michezo mingi ya ligi.
Kwa upande wa Yanga, Nado anaonekana kama chaguo sahihi katika mpango wao wa kuongeza nguvu kwenye winga, hasa kutokana na uzoefu wake ndani ya Ligi Kuu ya NBC na uthabiti wake katika msimu huu.
Msimu uliomalizika Yanga ilikuwa na changamoto eneo la washambuliaji wanaotokea pembeni baada ya sajili zilizotua kushinda kufikia matarajio.
Ni Pacome Zouzoua aliyekuwa akitumika zaidi pale Yanga inaposhambulia kupitia upande wa kushoto ambapo nae kwa nyakati tofauti alikosekana kutokana na changamoto ya majeraha.
Katika mchezo wa kuhitimisha msimu dhidi ya JKT Tanzania, Pacome alipata majeraha makubwa ambayo yanaweza kumuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Ni wazi katika dirisha hili Yanga itafanya usajili kuongeza nguvu kwenye eneo hilo la mawinga ili kurejesha umahiri wao wa kujenga mashambulizi kupitia mawinga.