Klabu ya Yanga iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Eswatini Justice "Figa" Figuareido kutoka klabu ya Chippa United.
Makubaliano binafsi kati ya Yanga na Figuareido tayari yamefikiwa huku mabingwa hao wa soka Tanzania Bara wakiwa pia wamekubaliana dau la usajili na klabu ya Chippa United.
Mchakato wa usajili wa mshambuliaji huyo ambaye pia anaweza kutumika kama kiungo mshambuliaji au winga, unatarajiwa kukamilishwa mapema wiki ijayo na mchezaji huyo kuungana na kikosi cha Yanga jijini Dar es salaam.
Figuareido pia anaitumikia timu ya Taifa ya Eswatini ambapo ameifungia mabao manne katika mechi 28. Akiwa na Chippa United msimu uliopita, alifunga mabao mawili na kutoa pasi 5 za mabao.
Kwa nini Figuareido?
Baada ya kuondoka Prince Dube, Yanga imehitaji kuongeza mshambuliaji ambaye ana sifa zinazoshabihiana au zaidi ya Dube ambaye mchango wake kwenye kikosi cha Yanga haukuwa kwenye mabao pekee.
Msimu uliopita Figa alihusika kwenye mabao 7 ligi kuu ya Afrika Kusini ambayo ina ushindani zaidi pengine kuliko ligi ya Tanzania Bara. Ni mchezaji anayeweza kufanya majukumu ya kiungo mshambuliaji kwa kuwatengenezea wenzake nafasi pale inapobidi.
Ujio wake akiungana na Laurindo Aurelio 'Depu' bila shaka utatengeneza uwiano baina yao kwani Depu ni aina ya mshambuliaji ambaye anategemea zaidi kutengenezewa nafasi ili afunge.
Kabla ya kusajiliwa na Chippa United, Figa aliitumikia Richards Bay akiifungia mabao matano na asisti 1. Figa pia aliifungia Eswatini mabao mawili katika katika kampeni ya kusaka tiketi ya kufuzu kombe la Dunia linalofikia tamati leo nchini Marekani kwa mchezo wa fainali kati ya Argentina dhidi ya Hispania.