Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga leo wanashuka uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuwakabili mabingwa wa Botswana Gaborone United katika mchezo wa mkondo wa pili hatua ya awali ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL).
Mtanange huo wa kuamua timu ya kufuzu raundi ya kwanza ya michuano hiyo, unatarajiwa kupigwa saa 1 usiku.
Wananchi wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na dhamira moja tu, kushinda mbele ya mashabiki wao na kukata tiketi ya hatua inayofuata.
Matokeo ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Botswana, yanafanya mchezo huo wa marudiano kuwa na umuhimu kwa kila timu Yanga ikiingia na faida ya bao la ugenini.
Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi amesema Gaborone United sio timu nyepesi hivyo wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na tahadhari kubwa.
Timu hiyo iliyonyesha hatari kubwa kwenye mipira ya kutenga kwenye mchezo uliopita, wakifunga bao lao kupitia aina hiyo ya mipira.
Katika mchezo huo Yanga inatarajiwa kutawala kama ilivyofanya mchezo wa kwanza huku Gaborone United pengine wakitumia mbinu zilezile za kuzuia huku wakisubiri nafasi yao kupitia mashambulizi ya kushitukiza, kona au faulo.
Ushindi wa aina yoyote utatosha kuivusha Yanga hatua inayofuata ingawa hata matokeo ya suluhu ya bila kufungana 0-0 pia yanawanufaisha Yanga kusonga mbele hatua inayofuata.