Winga Erick Mwijage jana aling'ara katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ambapo Yanga SC iliichapa St. George ya Ethiopia kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kudumisha urafiki baina ya timu hizo, ulimshuhudia Mwijage akionyesha ufundi mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga, na kutengeneza nafasi jambo lililomfanya kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki waliojitokeza dimba la Uhuru.
Yanga ilifunga bao lake kupitia kiungo mshambuliaji Albert Kagwanda akipokea pasi kutoka kwa Maxi Nzengeli kwenye dakika ya 60.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kiwango kikubwa cha Erick Mwijage kilimfanya Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, kumwagia sifa kedekede na kumtaja rasmi kuwa ana nafasi yake kwenye kikosi mchezo ujao wa ligi kuu ya NBC dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 10, 2026.
Mwijage mwenyewe alieleza kuwa siri ya kung'ara kwake ni kujituma mazoezini pamoja na kusikiliza maelekezo ya benchi la ufundi na miongozo kutoka kwa wachezaji wenzake wenye uzoefu mkubwa kikosini.