Msimu uliopita, kulikuwa na mawinga kadhaa waliotengeneza headlines kutokana na kasi, chenga na uwezo wao wa kuwatesa mabeki wa timu pinzani. Lakini kila walipokutana na Chadrack Boka, mara nyingi walikumbana na ukuta uliokuwa mgumu kuupenya.
Boka, beki wa kimataifa kutoka DR Congo anayechezea Young Africans SC, ameanza msimu wa 2026/27 akionyesha sura tofauti kabisa. Baada ya kukutana na ukosoaji katika baadhi ya nyakati msimu uliopita, beki huyo amerejea akiwa na kiwango kinachoonyesha kujiamini zaidi katika majukumu yake.
Miongoni mwa wachezaji waliowahi kukutana na mikiki ya Boka ni Ramadhan Chobwedo wa TRA United.
Chobwedo alijenga sifa kutokana na uwezo wake wa kucheza pembeni na kujaribu kuwasumbua mabeki kwa kasi na nguvu. Lakini alipokutana na Boka katika moja ya michezo ya mwishoni mwa msimu uliopita, mchezo ukawa na sura nyingine.
Boka hakumpa nafasi kubwa ya kufanya anachokifanya vizuri, kukimbia kuelekea eneo la hatari na kuleta madhara. Badala yake, alionekana kuwa karibu naye, akitumia nguvu na kasi yake kumzuia kupata nafasi ya kugeuka na kushambulia.
Libasse Gueye naye alikutana na Boka
Dabi ya Ngao ya Jamii pia ilitoa picha nyingine ya aina ya kazi ambayo Boka anaweza kufanya.
Winga wa Simba, Libasse Gueye, hakumaliza mchezo huo, lakini moja ya matukio yaliyoonyesha namna Boka alivyokuwa akifanya kazi ni pale Gueye alipolazimika kushuka na kumfuata Boka katika harakati za kuzuia mashambulizi.
Cha kufurahisha zaidi, pamoja na Gueye kujihusisha katika kumzuia Boka, bado beki huyo alipata nafasi ya kupandisha mpira na kutengeneza hatari.
Ndiyo Boka yuleyule aliyepiga krosi iliyozalisha bao pekee la ushindi wa Yanga katika mchezo huo, bao lililofungwa na Albert Kangwanda.
Kwa lugha nyingine, Boka hakuwa tu akifanya kazi yake nyuma; alikuwa pia akienda mbele na kuacha alama.
Boka wa msimu huu ni tofauti
Kinachovutia zaidi kuhusu Boka wa sasa ni namna anavyounganisha majukumu mawili.
Kwanza, ni beki anayehitaji kukabiliana na mawinga wenye kasi. Pili, anapopata nafasi, ana uwezo wa kupandisha timu na kushiriki katika ujenzi wa mashambulizi.
Nguvu, kasi, ukakamavu kwenye mipira ya kugombea na uwezo wa kurejea haraka kwenye nafasi yake ni baadhi ya vitu vinavyomfanya kuwa mchezaji anayehitaji umakini mkubwa kutoka kwa winga anayekabiliana naye.
Ampa wakati mgumu Zimbwe Jr
Kiwango anachoonyesha Boka kinaongeza ushindani ndani ya kikosi cha Yanga, hasa kwenye nafasi za pembeni.
Kwa sasa, Boka anaonekana kuwa chaguo la kwanza ingawa kocha Manqoba Mangqithi ameendelea na utaratibu wa kumpa nafasi kila mchezaji kwa kuzingatia mahitaji ya mechi.
Boka amekuwa akitumika zaidi kwenye mechi zenye ushindani mkubwa na athari yake imeonekana akiwa amefunga mabao mawili kwenye ligi pamoja na kutoa pasi mbili za mabao mapaka sasa.
Katika msimu ambao wengi walidhani Mcongoman huyo angepewa mkono wa kwaheri, amerejea akiwa mchezaji tofauti ambaye sasa kila shabiki wa Yanga anafurahia kumuona uwanjani.