Kinda wa Yanga SC, Ibrahim Kazimoto, ameanza kuonyesha dalili za kuwa moja ya vipaji vinavyoweza kuwa na nafasi kubwa ndani ya kikosi cha kwanza, baada ya kiwango chake kuwavutia makocha wa timu hiyo.
Kocha wa timu za vijana za Yanga, Mohamed Badru, amesema kocha wa kikosi cha kwanza, Manqoba Mngqithi, amevutiwa na uwezo wa Kazimoto tangu alipopandishwa kutoka timu ya U-20.
Badru amesema Kazimoto ana baadhi ya sifa zinazohitajika katika soka la kisasa, ikiwemo nguvu, kasi, uwezo wa kupambana na uelewa wa kiufundi, jambo lililompa nafasi ya kuanza kuonekana katika kikosi cha kwanza.
Kocha huyo amesema ilikuwa sehemu ya mpango wake tangu alipoanza kufanya kazi Yanga, akilenga kuona angalau mchezaji mmoja au wawili kutoka U-20 wakipenya kikosi cha kwanza msimu huu.
Hata hivyo, Badru anaonya kuwa safari ya Kazimoto bado ndiyo inaanza. Anahitaji kuendelea kufanyiwa kazi kiufundi, kuvumilia ushindani na kujifunza kutoka kwa wachezaji wenye uzoefu ili kufikia kiwango cha juu zaidi.
Kazimoto ambaye kwenye timu ya vijana alikuwa akitumika kama beki wa kati, alicheza dakika zote 90 mchezo wa ligi kuu dhidi ya Geita Gold huku pia akitumika kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya St George.