Mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Yanga SC, wanatarajiwa kushuka dimbani nchini Mauritius kati ya tarehe 16 na 18 Oktoba 2026 kumenyana na CFFA FC katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ingawa timu ya CFFA FC inatokea nchini Madagascar, italazimika kutumia viwanja vya Mauritius kama uwanja wao wa nyumbani kwa ajili ya mchezo huo baada ya Madagascar kukosa uwanja unaokidhi vigezo vya CAF.
Hatua hii unaweza kusema ni habari njema kwa Yanga kwani licha ya kuwa ugenini, wapinzani wao nao ni kama watakuwa ugenini katika mchezo huo wa kwanza.
Baada ya mtanange huo wa kwanza ugenini, miamba hiyo ya Jangwani itarudi nyumbani Tanzania kukamilisha ratiba katika mchezo wa marudiano utakaopigwa kati ya tarehe 23 na 25 Oktoba 2026.
Mshindi wa jumla katika mechi hizo mbili atakwenda moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Msimu huu Yanga imeweka malengo ya angalau kufika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.