Yanga wamekubali matokeo kupoteza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba uwanja wa Uhuru juzi lakini yapo matukio ambayo kama yangefanyika upande wa watani zao Simba halafu wakapoteza mchezo pengine mpaka leo mijadala ingekuwa mikali kila kona.
Tukio la rafu mbaya aliyochezewa Duke Abuya na winga wa Simba Libasse Gueye ni moja ya matukio mabaya yaliyoonekana kwenye mchezo huo.
Rafu kama ndio iliyosababisha Stephane Aziz Ki akakosa mchezo dhidi ya Simba baada ya kupewa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold baada ya usaidizi wa FVS.
Kwenye mchezo wa juzi tukio la rafu ya Gueye ni kama llifumbiwa macho, hata kama benchi la ufundi la Yanga hawakuliona mapema kuomba 'review' maafisa wa FVS walikuwa na nafasi ya kumsaidia mwamuzi Ahmed Arajiga kun'gamua tukio hilo.
Sitaki kuamini siku ikitokea mchezaji akafanyiwa rafu mbaya ya kuhatarisha maisha yake FVS hawatajali kwa kuwa benchi la ufundi la timu husika hawakuona?
Ni rafu mbaya ambayo ilistahili kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa Gueye, mchezaji huyo alikuwa na bahati kumaliza dakika zote 90.
Kwa kuwa tukio hilo halikuonekana na waamuzi, basi Kamati ya saa 72 inapaswa kuchukua hatua kwa kutoa adhabu stahili kwa mhusika.
Tukio hilo limepelekea Abuya kuumia na anaweza kuwa nje kwa zaidi ya wiki mbili akiuguza majeraha.