Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi ameweka wazi kuwa kikosi chake kimejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya CFFA ya Madagascar.
Mchezo huo utapigwa kesho Jumamosi Oktoba 17 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.
Yanga imepata faida ya kucheza mechi zote mbili nyumbani baada ya wapinzani wao CFFA kukosa uwanja unaokidhi vigezo vya CAF nchini mwao na hivyo kuridhia kucheza mechi yao ya nyumbani hapa nchini.
Akizungumza baada ya kikosi chake kukamilisha mazoezi hapo jana, Manqoba alisema wanatambua ugumu ulioko mbele yao kwani hakuna mechi nyepesi katika hatua hii ya mtoano.
Mngqithi, amesema hawapaswi kuwadharau wapinzani wao kutokana na nidhamu na mipango yao ya mchezo, akisisitiza kuwa timu yake inapaswa kujiandaa vizuri ili kupata matokeo mazuri katika mechi hizo mbili.
“Akili yetu kwa sasa ni kuangalia mechi zetu mbili zinazofuata. Tunakutana na CFFA, ambayo si timu nyepesi. Wameshinda mechi ya kwanza wakiwa nyumbani, ingawa walikuwa mbali na kwao Madagascar”
“Kama waliweza kufanya hivyo, hata wanapoamua kucheza hapa wanaweza kuonyesha ubora wao. Hii si timu inayokata tamaa; wanacheza kwa nidhamu kubwa."
“Tunatakiwa kujipanga kwa kuzingatia ubora wao na kuhakikisha tunaweza kuwafungua na kuwalazimisha kufanya makosa. Hata wanapokuwa ugenini, wana mpango tofauti. Tunahitaji kushinda mechi hizi mbili, tukitambua kuwa haitakuwa rahisi,” alisema
Baada ya ugumu waliopata kwenye hatua iliyopita wakilazimika kusubiri mechi ya mkondo wa pili kutinga raundi ya kwanza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gaborone United, kuelekea mchezo huo Yanga imepania kumaliza biashara mapema.
Hata hivyo ni wazzi haitakuwa mechi nyepesi kwani hata wapinzani wao CFFA wamekuja wakiwa na dhamira ya kusaka ushindi na kuandika historia ya kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.