Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga SC, Ali Kamwe, amepongeza hatua ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya kuanzisha rasmi utaratibu wa kuwapima wachezaji ili kubaini matumizi ya dawa za kusisimua miili na kuongeza nguvu michezoni (doping).
Hatua hiyo ilitangazwa na Rais wa TFF, Wallace Karia, baada ya kuibuka kwa mijadala na shutuma mbalimbali juu ya uwezekano wa uwepo wa matumizi ya mbinu mbadala na vitu vilivyopigwa marufuku ili kuongeza uwezo wa miili uwanjani kwenye soka la ndani.
Akizungumzia uamuzi huo, Kamwe ameeleza kuwa hatua hiyo imekuja kwa wakati sahihi na ni ukombozi mkubwa kwa soka la Tanzania.
Alibainisha kuwa mchakato huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda afya za wachezaji wenyewe, kulinda vipaji na taaluma zao dhidi ya madhara ya muda mrefu ya kemikali hizo, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na uwanja sawa wa ushindani wa haki na uadilifu viwanjani.
Katika tangazo lake la awali, Rais Karia alifafanua kuwa TFF imeanza mchakato wa kuunda kamati maalum itakayoshirikiana bega kwa bega na mamlaka za serikali ili kusimamia ipasavyo vipimo hivyo na kuhakikisha kanuni za kupambana na doping zinazingatiwa kikamilifu kulingana na miongozo ya kimataifa ya Shirika la Kupambana na Doping Duniani (WADA).