Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga SC, wanatajwa kuwa mbioni kuemrejesha kikosini kocha raia wa Ujerumani mwenye asili ya Bosnia, Sead Ramovic, ikiwa ni miezi michache tu tangu alipoondoka klabuni hapo kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria.
Kurejea kwa Ramovic kunatajwa kama mkakati wa Yanga kusimika nidhamu ya chuma kikosini na kuendeleza falsafa ya soka la kisasa la kushambulia.
Kabla ya kuingia kwenye rada za soka la Afrika Mashariki, Ramovic alijizolea sifa kubwa nchini Afrika Kusini akikiwasha na klabu ya TS Galaxy kwa misimu mitatu (2021–2024). Huko, aligeuka kuwa 'mkombozi' baada ya kuipandisha timu hiyo kutoka mkiani na kuifanya tishio kwenye Top 8 ya Ligi Kuu ya PSL.
Zaidi ya mbinu uwanjani, Ramovic alijenga sifa ya kuwa kocha wa biashara. Chini yake, TS Galaxy ilikuza na kuuza wachezaji nyota zaidi ya 12 kwenda klabu kubwa kama Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates, huku akiiingizia klabu hiyo kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 5 za Kitanzania.
Aliondoka nchini humo mwezi Novemba 2024 baada ya kuchoka 'kubomoa na kujenga' kila msimu kufuatia uuzaji holela wa wachezaji wake tegemeo.
Baada ya kuondoka TS Galaxy, Yanga walimnasa haraka Novemba 2024 ili kuziba pengo la Miguel Gamondi. Hata hivyo, mapenzi yake na Wananchi yalikuwa ya "muda mfupi". Baada ya kuongoza michezo sita tu ya kimashindano, Ramovi alitimka ghafla mwezi Februari kufuata ofa nono zaidi kutoka kwa miamba ya soka ya Algeria, CR Belouizdad.
Huko Algeria, rekodi za Ramovic hazikuwa mbaya kiufundi. Aliongoza klabu hiyo katika michezo zaidi ya 55, akivuna wastani mkubwa wa pointi 1.96 kwa kila mchezo na kuifikisha timu hiyo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC).
Timu yake ilitawala mechi kwa soka la pasi nyingi likifikia wastani wa umiliki wa asilimia 64. Hata hivyo, dhoruba ilimkumba kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwenye ligi ya ndani ambapo timu ilishuka hadi nafasi ya saba, sambamba na migogoro ya chinichini na Bodi ya Wakurugenzi.
Hali hiyo ilichangiwa pia na klabu hiyo kushindwa kumlipa mshahara wake kwa miezi minne, jambo lililopelekea mgogoro mkubwa na hatimaye kuamua kuvunja mkataba wake.
Uongozi wa Yanga chini ya Rais Hersi Said umevutiwa na uwezo wa Ramovic wa kusimamia nidhamu na mbinu zake za kisasa. Kwa kuwa sasa yuko huru (free agent), Yanga imeona hakuna haja ya kufanya majaribio na kocha mgeni asiyejua mazingira ya klabu hiyo, bali wamemrudisha mtu ambaye tayari anajua uzito wa nembo ya klabu.
Ramovic anarejea Jangwani huku kibarua chake kikuu kikiwa ni kulinda ubingwa wa ndani na kuhakikisha Yanga inafika mbali zaidi katika ligi ya mabingwa.