Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga SC, Peter Shalulile, ameendeleza kasi yake ya kutikisa nyavu baada ya kuibeba klabu hiyo katika michuano ya ndani na kimataifa msimu huu.
Nyota huyo wa kimataifa wa Namibia amefunga mabao sita kwenye Ligi Kuu ya NBC na bao moja katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), akihusika moja kwa moja kwenye mabao saba ya timu hiyo.
Kasi kuzifumania nyavu ya Shalulile imezidi kuwapa burudani mashabiki wa mabingwa hao watetezi. Katika Ligi Kuu ya NBC, ameshazitungua timu za Namungo FC, JKT Tanzania, Fountain Gate, Simba SC, Mashujaa SC, na Kagera Sugar.
Mabao hayo sita yanamfanya kushika nafasi ya pili kwenye chati ya wafungaji bora, akimkaribia mshambuliaji wa Fountain Gate, Anuary Jabir, mwenye mabao saba.
Kama hiyo haitoshi, Shalulile ameonyesha ukongwe wake kwenye anga la kimataifa baada ya kufungua akaunti yake ya mabao ndani ya Yanga kwenye michuano ya CAF Champions League, akifunga bao muhimu dhidi ya Gaborone United.
Bao hilo liliifanya Yanga kufikisha jumla ya mabao 21 katika historia ya ushiriki wake kwenye michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu barani Afrika. Idadi hiyo ya mabao sasa imefika 29.
Wakati Yanga inamsajili kutoka Mamelodi Sundowns wapo waliobeza usajili huo wakiamini muda wake wa kun'gara umemalizika.
Hata hivyo tangu atue kwa Wananchi ni kama amezaliwa upya kwani msimu wake wa mwisho na Mamelodi Sundowns alifunga mabao matatu pekee.
Kama hatakumbwa na changamoto ya majeraha, Shalulile anatabiliwa atakuwa miongoni mwa washambuliaji watakaomaliza msimu na idadi kubwa ya mabao kama sio kuibuka mfungaji bora