Klabu ya Yanga SC imeendelea kuimarisha benchi lake la ufundi kwa kumpokea Kocha Maahier Davids, ambaye sasa atakuwa sehemu ya makocha wasaidizi wa kikosi hicho kinachojiandaa kukabiliana na changamoto za mashindano ya ndani na kimataifa.
Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya mabingwa hao wa Tanzania ya kuongeza nguvu katika benchi la ufundi, hasa wakilenga kufanya vizuri katika kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Maahier ni mdogo wa Kocha Mkuu wa Yanga, Fadlu Davids, hivyo ujio wake unawaunganisha tena wawili hao katika majukumu ya kusimamia na kuendeleza kikosi. Inadaiwa kuwa amevutiwa na mazingira ya klabu hiyo, jambo lililorahisisha safari yake ya kujiunga na Wananchi.
Kwa upande wa taaluma, Maahier si mgeni katika ulimwengu wa ukocha. Ana leseni ya UEFA A Licence, inayompa sifa ya kufanya kazi katika ngazi ya juu ya soka, huku akiwa na uzoefu wa kutosha katika vilabu mbalimbali barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.
Ushirikiano wake na Fadlu Davids pia una historia ndefu. Wawili hao waliwahi kufanya kazi pamoja mwaka 2016, kipindi ambacho Fadlu alipewa jukumu la kuwa Kocha Mkuu wa muda wa Maritzburg United, iliyokuwa ikijulikana pia kama Durban City FC, baada ya kuondoka kwa Ernst Middendorp.
Katika safari yake ya ukocha, Maahier amepata nafasi ya kufanya kazi na timu kadhaa zikiwemo Orlando Pirates, Maritzburg United na Free State Stars za Afrika Kusini. Pia amewahi kuwa sehemu ya benchi la Saint George, inayojulikana kama Kidus Giorgis ya Ethiopia, Cape Umoya United FC na timu za vijana za Ajax Cape Town.
Uzoefu wake hauishii katika soka la Afrika pekee. Maahier pia amewahi kushirikiana na kocha maarufu Pitso Mosimane katika vilabu mbalimbali, ikiwemo Al-Ahli SFC na Abha Club za Saudi Arabia, Al-Wahda FC ya Falme za Kiarabu pamoja na Esteghlal FC ya Iran.
Kuingia kwake katika benchi la ufundi la Yanga kunafanya idadi ya makocha wasaidizi kufikia watatu. Hata hivyo, kuna uwezekano wa mabadiliko mengine kufanyika, kufuatia taarifa zinazomhusisha kocha Simo Dladla na klabu ya Richards Bay FC ya Afrika Kusini, ambayo inadaiwa kuanza mazungumzo naye.