Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Simo Dladla, ameandika ujumbe maalumu wa kuwaaga Wananchi, akitoa shukrani kwa uongozi wa klabu hiyo kwa nafasi aliyopewa ya kuhudumu katika benchi la ufundi, huku akithibitisha kuondoka kwake kuelekea Richards Bay FC ya Afrika Kusini.
Dladla, ambaye pia aliwahi kukabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha Yanga kwa muda baada ya kuondoka kwa Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi, amesema anajivunia kipindi alichokitumikia kikosi hicho cha Jangwani.
Katika ujumbe wake aliouelekeza kwa Rais wa Yanga, Makamu wa Rais, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Dladla amesema kufanya kazi katika klabu kubwa kama Yanga ni heshima ya kipekee katika maisha yake ya ukocha.
"Ninaandika ujumbe huu kutoa shukrani zangu za dhati kwa nafasi niliyopewa ya kuitumikia Young Africans SC kama Kocha Msaidizi wa Kwanza, pamoja na imani niliyoonyeshwa nilipokabidhiwa jukumu la kuwa Kocha Mkuu wa Muda.
"Kufanya kazi katika klabu kubwa yenye hadhi kama hii kumekuwa heshima kubwa kwangu na moja ya hatua muhimu katika maisha yangu ya ukocha," amesema Dladla.
Afunguka sababu za kuondoka
Akizungumzia uamuzi wake wa kuachana na Yanga, Dladla amesema mabadiliko ya mfumo na falsafa ya ufundishaji ndani ya klabu hiyo yamechangia uamuzi wake wa kutafuta changamoto mpya.
Amesema anaamini ni muhimu kumpa Kocha Mkuu mpya na wasaidizi wake uhuru wa kutekeleza mipango yao bila kuingiliwa, jambo ambalo litasaidia timu kufikia malengo yake.
"Kwa kuwa klabu inaingia katika mwelekeo mpya wa kiufundi, naamini ni kwa manufaa ya timu kumpa Kocha Mkuu mpya na benchi lake la ufundi uhuru kamili wa kutekeleza falsafa yao.
"Kutokana na hilo, nimekubali changamoto mpya ya kuwa Kocha Mkuu wa Richards Bay FC nyumbani kwetu Afrika Kusini," amesema.
Yanga yabaki moyoni mwake
Licha ya kuondoka, Dladla ameonyesha mapenzi makubwa kwa Yanga, akisisitiza kuwa klabu hiyo itaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha yake.
Amewashukuru viongozi kwa ushirikiano, weledi na mapokezi mazuri aliyoyapata katika kipindi chote alichokuwa jijini Dar es Salaam.
"Nawashukuru kwa weledi, msaada na upendo mlionionyesha katika kipindi changu nilichokuwa Dar es Salaam.
"Yanga SC itaendelea kuwa na nafasi ya pekee moyoni mwangu, na nipo tayari kutoa huduma zangu endapo klabu itanihitaji tena siku zijazo," amesema.
Dladla anarejea Richards Bay akiwa anaifahamu vizuri klabu hiyo, baada ya kuwahi kuifundisha kati ya mwaka 2020 na 2021.