Kocha mpya wa Yanga Fadlu Davids ameanza vyema majukumu yake ya kuwatumikia Wananchi leo akikiongoza kikosi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliopigwa uwanja wa Ushirika, Moshi.
Haukuwa ushindi tu kwa Yanga bali pia kikosi kilionyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji kwani licha ya kuwa ugenini Yanga ilitawala mchezo huo kwa muda mwingi na pengine walistahili kuondoka na ushindi mnono zaidi.
Alikuwa ni Cheick Ibrahim Toure aliyeanza kutikisa nyavu kwenye dakika ya 30 akimalizia krosi ya Mudathir Yahya.

Bao hilo liliipeleka Yanga mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Polisi Tanzana walikianza kwa nguvu wakisaka bao la kusawazisha hata hivyo ilikuwa ni Yanga iliyoongeza bao la pili dakika ya 75 kupitia Peter Shalulile aliyeweka mpira kambani akimalizia pasi ya Clement Mzize aliyekuwa bora sana kwenye mchezo huo.
Pengine Yanga ilikuwa na nafasi ya kupata mkwaju wa penati mapema kipindi cha pili baada ya Shalulile kufanyiwa madhambi katika tukio ambalo lilionekana kuwa ndani ya eneo la hatari lakini baada ya mapitio ya FVS, mpira ulitolewa nje ya 18 na kuwa pigo la adhabu.
Dakika 90 za mchezo huo zikawahakikishia Wananchi wakiondoka na alama zote tatu na sasa wakifika alama 28, alama mbili nyuma ya watani zao Simba ambao kesho watashuka dimba la Isamuhyo kuikabili JKT Tanzania.