Kiungo wa Yanga Maxi Nzengeli anaendelea na mazoezi mepesi huku hatma yake ikitarajiwa kufahamika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ujao.
Maxi anasumbuliwa na jeraha la goti taarifa za awali zikibainisha kuwa anapaswa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema hatma ya nyota huyo raia wa Congo itafahamika baada ya wiki nne kama anarejea kikosini au atahitaji kufanyiwa upasuaji.
"Maxi anaendelea na mazoezi mepesi huku madaktari wakiangalia hali yake. Baada ya vipimo vya awali, alihitaji angalau wiki 6 za uangalizi kuona kama atapona bila ya kufanyiwa upasuaji au la."
"Katika kipindi cha wiki nne tutafahamu kama anaweza kurejea kwenye majukumu yake bila ya upasuaji au aende kwenye upasuaji unaoweza kumuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu zaidi," alisema Kamwe.
Maxi aliyeanza msimu vyema, alipata majeraha kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar, mchezo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Msimu huu amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Yanga akiondoka na tuzo sita za nyota wa mchezo katika mechi 10 za lig lizocheza
Ameifungia Yanga mabao matatu na kutoa pasi tatu za mabao kwenye ligi.