Yanga SC imeanza vibaya kampeni yake ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa MC Alger ya Algeria mbele ya mashabiki wake nyumbani.
Katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi B, Yanga ilijikuta ikipoteza matumaini ya kuambulia angalau pointi moja baada ya mshambuliaji wa MC Alger, Soufiane Bayazid, kufunga bao la ushindi dakika ya 90.
Bayazid aliunganisha kwa kichwa mpira wa kona na kuzima matumaini ya mashabiki wa Wananchi katika dakika za mwisho za mchezo.
Yanga iliuanza mchezo huo taratibu kipindi cha kwanza wakitengeneza nafasi adimu moja kupitia kwa Yao Kouassi ambaye shuti lake liligonga mwamba.
Kipindi cha pili ni Yanga iliyotawala zaidi huku MC Alger wakitumia mashambulizi ya kushitukiza wakiwa hatari zaidi kwenye mipira ya kutenga.
Dakika za lala salama Seleman Mwalimu alikaribia kusawazisha kama sio mlinda lango wa MC Alger kuondosha shuti ndani ya 18.
Sio matokeo yaliyotarajiwa na Wananchi lakini ni wazi ulikuwa mchezo wa kimbinu zaidi MC Alger wakinufaika na kuondoka na alama tatu ugenini.
Yanga sasa itahitaji kwenda kuzirejesha alama hizi kwenye mechi ya ugenini ili kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua inayofuata.
Wananchi wamepoteza nyumbani lakini ndio kwanza hatua ya makundi imeanza, lolote linaweza kutokea.