Licha ya kuanza kwa mguu mbaya katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) msimu wa 2026/2027, Kocha Mkuu wa Yanga SC, Fadlu Davids, amesisitiza kuwa bado ana imani kubwa na kikosi chake katika harakati za kufuzu hatua ya robo fainali.
Wananchi walikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya MC Alger ya Algeria katika mchezo wa kwanza wa Kundi B, uliochezwa Jumamosi, Novemba 28, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Bao la dakika ya 90 lililofungwa na Soufiane Bayazid liliwanyima Yanga nafasi ya kuambulia pointi mbele ya mashabiki wao.
FADLU HAJAKATA TAMAA
Akizungumza baada ya kikosi hicho kurejea Dar es Salaam, Fadlu amesema licha ya kupoteza mchezo huo, ameridhishwa na namna wachezaji wake walivyotekeleza maelekezo ya benchi la ufundi, hususan katika kipindi cha pili.
Kocha huyo ameeleza kuwa Yanga ilionyesha uwezo mkubwa wa kutawala mchezo na kuwabana wapinzani katika eneo lao la uwanja, huku akibainisha kuwa yapo mambo machache yanayohitaji kufanyiwa marekebisho.
“Kuna mambo madogo tunayohitaji kurekebisha, lakini wachezaji walijitahidi kutekeleza maelekezo. Katika kiwango hiki, tofauti kati ya timu huwa ndogo sana,” amesema Davids.
ROBO FAINALI BADO IPO MACHONI
Fadlu amesisitiza kuwa kipigo hicho hakijabadilisha malengo ya Yanga katika michuano hiyo, akieleza kuwa anaendelea kuwa na imani na ubora wa kikosi chake pamoja na kazi inayofanywa na benchi la ufundi.
Kwa kocha huyo, kupoteza mchezo mmoja hakumaanishi mwisho wa safari, kwani bado kuna michezo mitano ya kupambania nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali.
Jukumu kubwa kwa Wananchi ni kurejesha morali, kurekebisha makosa yaliyojitokeza na kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika michezo inayofuata.