Nahodha wa Yanga Ibrahim Ajib amesema watahakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Biashara Fc ili kuweka hai matumaini ya kutwaa taji hilo
Yanga itashuka dimba la Taifa Alhamisi ijayo, Januari 31 kuikabili Biashara United katika mchezo wa kombe la FA (ASFC) raundi ya tano
Ajib aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa nahodha wa kikosi cha Yanga amesema anatambua mashabiki wa timu hiyo wamesikitishwa na matokeo ya kupoteza michezo miwili iliypita lakini amewataka wasife moyo kwani wachezaji wameahidi kuirejesha furaha yao
"Baada ya kukosa kombe la Mapinduzi na SportPesa, matumaini yetu sasa yamebaki katika ligi kuu na kombe la FA"
"Lengo letu ni kuhakikisha tunashinda mataji haya. Tunawaomba mashabiki wetu waje watuunge mkono kwenye mchezo dhidi ya Biashara United, hatutawaangusha," amesema Ajib
Baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo, Yanga inahitaji kushinda mchezo dhidi ya Biashara United ili kurejesha morali ya mashabiki ambao baadhi wameanza kuwa na hofu juu ya uwezo wa timu yao
Matokeo tofauti na ushindi huenda yakaiweka Yanga kwenye wakati mgumu hasa ikizingatiwa baada ya siku tatu itacheza na Coastal Union katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa dimba la Mkwakwani mkoani Tanga