Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa KMC mabao 2-1 katika mchezo mkali uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa leo
KMC ilitangulia kufunga kwenye dakika ya 17 kupitia kwa mshambuliaji Mohammed Rashidi anayecheza kwa mkopo kutoka klabu ya Simba
Mo Rashid alifunga bao hilo baada ya kuwazidi maarifa Thabani Kamusoko na Gadiel Michael waliokuwa wakimzuia baada ya KMC kufanya shambulizi ya kushitukiza
Hata hivyo Yanga ilirejea mchezoni kwenye dakika ya 37 baada ya Papi Tshishimbi kuisawazishia kwa mpira wa kichwa akimalizia krosi murua ya Gadiel Michael
Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mwinyi Zahera kwenye kipindi cha pili kwa kuwatoa Thabani Kamusoko na Deus Kaseke na nafasi zao kuchukuliwa na nahodha Ibrahim Ajib na Amissi Tambwe yaliinufaisha Yanga kwenye dakika ya 67 baada ya krosi murua ya Ajib kutua kichwani kwa beki wa KMC Ally Ally na kuiandikia Yanga bao la pili
Baada ya 'assist' hiyo, Ajib alivua kitambaa chake cha unahodha na kuwaonyesha mashabiki waliokuwa wakishangilia bao hilo ikiwa ni ishara ya kuwafahamisha kuwa nahodha yuko dimbani
Wakati mchezo ukielekea ukingoni KMC ilifanya mashambulizi kadhaa ya hatari langoni kwa Yanga lakini uimara wa mlinda lango Klaus Kindoki uliihakikishia Yanga kuondoka na alama zote tatu
Ushindi huo umeendelea kuikita Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 67