Yanga inatarajiwa kuanza kutumia uwanja wa CCM Kirumba kwa michezo yake ya ligi wakati uwanja wa Taifa utakapofungwa baada ya mchezo wa Jumapili wa kusaka tiketi ya kutinga fainali ya AFCON 2019 kati ya Stars dhidi ya Uganda
Mashabiki wa Yanga wa Mwanza wametakiwa kuipokea na kuiunga mkono timu yao wakati wote itakapokuwa jijini humo
Meneja wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema anaamini watapata mapokezi mazuri kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo hapo Mwanza
"Mara zote tunapokwenda Mwanza tumekuwa tukipokelewa vizuri sana. Muamko wa mashabiki ni mkubwa sana na naamini hali itakuwa hivyo kwa kipindi chote ambacho tutakuwa tukicheza katika dimba la CCM Kirumba," amesema
Yanga inatarajiwa kutumia uwanja wa CCM Kirumba kwa michezo yake yote ya nyumbani ambayo itapigwa mwezi wa nne.
Wiki ijayo March 30 itachuana na Alliance katika mchezo wa robo fainali ya kombe la FA, mchezo ambao itakuwa ugenini
Uwanja wa Taifa utafungwa March 25 kupisha ukarabati tayari kutumika kwenye michuano ya AFCON U17 inayofanyika nchini kuanzia April 14-28
Yanga, Azam Fc, Simba, African Lyon, KMC na Ruvu Shooting ambazo zinatumia viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex, zimetakiwa kutafuta viwanja vingine kwa kipindi chote amacho viwanja hivyo vitakuwa vimefungwa
Wakati Yanga ikichagua uwanja wa CCM Kirumba, watani zao Simba wameelekea uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, Azam FC itatumia uwanja wa Nyamagana Mwanza, Ruvu Shooting itaendelea kutumia uwanja wa Mabatini, African Lyon uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha