Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Dismas Ten amesema licha ya changamoto zilizopelekea kufa kwa mradi wa Jarida la Yanga, klabu ilinufaika kutokana na mradi huo
Mwaka 2017 Yanga ilianzisha mradi wa kuchapisha Jarida ambalo lilipaswa kutoka kila mwezi. Hata hivyo Jarida hilo lilitoka mara moja na mradi kushindwa kuendelea
Ten amesema katika toleo lake la kwanza, nakala 500 zilichapishwa ambapo nakala 440 ziliuzwa na nakala 30 zikitolewa bure kwa wadau maalum wa klabu ya Yanga huku nakala 30 zikiharibika
"Katika hizo 470 nakala 440 tu ndiyo zilizouzwa huku 30 zikitolewa kwa heshima (Kutoa heshima-complimenatary) kwa viongozi wa serikali ambao ni mashabiki wa Young African Club, makampuni kwa lengo la kulitangaza jarida na kutafuta matangazo," ameandika Ten katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram
"Kwa kuwa mtaji ulikuwa mdogo na nakala zilizochapwa na kuuzwa kuwa chache hivyo mauzo hayakuwa makubwa sana japo yalileta faida kwa namna moja ama nyingine"
Baada ya kutumia vitu vya kukodi au kuazima kwa muda mrefu, kupitia mauzo ya Jarida hili, kwa mara ya kwanza idara ilifanikiwa kununua Kamera mbili za kisasa pamoja na vifaa vingine vidogo ambavyo sasa vinasaidia baadhi ya mambo muhimu katika idara yetu ikiwemo uzalishaji wa kipindi chetu cha Yanga Tv pia kupiga picha na matukio mengine ambayo huwekwa kwenye website na mitandao yetu ya kijamii"
Aidha Ten amefafanua kuwa mradi huo haukufadhiliwa na Yanga moja kwa moja, bali ulitokana na michango ya wadau wake kupitia makundi ya WhatsApp
"Kwa ushirikiano na umoja wa makundi ya WhatsApp ya Yanga (yapatayo 80 wakati huo) tulifanikiwa kusajili jarida letu, Habari Maelezo na sehemu nyingine husika kwa mujibu wa Sheria na Taratibu za nchi"