Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amewashukuru wapenzi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika Harambee ya kuichangia timu hiyo ambayo ilihitimishwa juzi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam
Mwakalebela amesema malengo waliyokuwa wamejiwekea yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na anaamini msimu ujao watairejesha furaha ya mashabiki iliyopotea kwa takribani misimu miwili
Amesema wamejipanga kurejesha hadhi na heshima ya Yanga ambayo ilitetereka
"Tunawashukuru Wanayanga wote, mafanikio yaliyoonekana kwenye Harambee yetu, umoja na ushirikiano kutoka kwa makundi yote ya mashabiki na wanachama, ni vitu vilivyotupa nguvu viongozi kwani tunaamini sasa hakuna cha kutukwamisha," amesema
"Tumejipanga kuweka historia si katika ligi tu, kila mashindano tutakayoshiriki msimu ujao tutakuwa na moto uleule"
"Yanga ile ambayo wengi walikuwa wakiitaka sasa inarudi msimu ujao. Kila kitu kinakwenda vizuri, tutashirikiana na hakika tutashinda"
cutKuhusu fedha zilizopatikana, Mwakalebela amesema watalipa madeni ya wachezaji na wataendelea kukiimarisha kikosi kwa kusajili wachezaji mahiri zaidi
Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa Mh Anthony Mavunde juzi alitangaza kuwa Yanga ilikusanya jumla ya Milioni 920 tangu kuanza kwa zoezi la kuichangia timu hiyo
Katika Harambee ya kubwa kuliko Yanga ilikusanya zaidi ya Milioni 650 fedha zilizochangishwa ukumbini
Fedha hizo hazijumuishi mapato yaliyopatikana kutokana na tukio lenyewe ambalo kiingilio kilikuwa kati ya Milioni 10 na Elfu 20