Miongoni mwa mambo ya kushangaza kutoka kwa baadhi mashabiki wa Yanga ni hili la kupima uwezo wa kocha kupitia michezo ya kirafiki
Kuna mambo kadhaa ambayo mashabiki wa Yanga wanapaswa kufahamu
Kwanza mafanikio ya timu yoyote hayapatikani kwa siku moja, mara chache hutokea lakini hiyo inaitwa bahati
Hata katika maisha ya kawaida mafanikio yanajengwa, unaweka juhudi, maarifa, uvumilivu baadae mambo yanatokea
Ni hivyo hivyo kwenye soka, hata hao Simba ambao leo wanatamba kuliteka soka la Tanzania, iliwachukua zaidi ya miaka mitano kujisahihisha
Inashangaza kuona baadhi ya mashabiki leo wanasema kocha Mwinyi Zahera hafai kwa sababu tu timu haichezi vizuri kwenye michezo ya kirafiki
Wamesahau ni huyu huyu Zahera aliyekuwa na kikosi 'dhaifu' msimu uliopita na kufanikiwa kumaliza nafasi ya pili tena baada ya kufanyiwa 'figisu' nyingi
Zaidi ya nusu ya wachezaji wa Yanga ni wapya na ni hao hao wanaotegemewa kwenye kikosi cha kwanza
Wengi wetu tunakubaliana, baadhi wameonyesha uwezo kwa mchezaji mmoja mmoja lakini kinachokosekana ni muungano wa kitimu
Muunganiko huo utapatikana baada ya wachezaji kuifahamu filosofia ya Mwalimu na wao kuzoeana
Kazi hiyo inaonekana kwani timu imeendelea kuimarika siku hadi siku
Ni bahati mbaya msimu huu michuano ya ligi ya mabingwa imeanza kipindi ambacho Yanga haikuwa tayari
Muda wa maandalizi ulikuwa mdogo huku timu ikimkosa kocha Mkuu na baadhi ya wachezaji waliokuwa wakishiriki michuano ya Afcon
cutLakini licha ya changamoto hizo, Yanga haikuwa na mwenendo mbaya sana, imefungwa mechi moja tu ya kirafiki na walionyesha ushindani kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
Nadhani mashabiki wanaohoji uwezo wa Zahera wakati huu wanakosea, pengine wavute subira angalau baada ya mechi tano za ligi wanaweza kupata picha mahali ilipo Yanga
Huu ni wakati wa Wanayanga kuiunga mkono timu yao na kuacha kuponda juhudi zinazofanywa katika kuiimarisha timu, ni suala la muda tu mbivu na mbichi zitafahamika
Kwa sasa Wanayanga wafikirie zaidi mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
Matokeo ya michezo ya kirafiki huwa hayana maana yoyote kwa kuwa makocha huitumia michezo hiyo kujaribu mbinu mbalimbali wanazofundisha mazoezini
Na ndio maana Zahera amekuwa akitumia vikosi tofauti tofauti kwenye michezo hiyo, jambo ambalo hawezi kufanya kwenye ligi na michuano ya Kimataifa