Jumapili Yanga ilikamilisha mechi tatu za ligi kuu ya Vodacom ikijikusanyia alama nne baada ya kushinda mechi moja, kutoka sare na kufungwa mechi moja
Katika mechi hizo Yanga imefunga mabao manne, mshambuliaji David Molinga akifunga mabao mawili na mengine yakifungwa na Mrisho Ngasa na Abdulaziz Makame
Msimu uliopita Yanga ikiwa na mshambuliaji Heritier Makambo, katika mechi tatu za kwanza ilishinda zote
Ilianza kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1, Makambo akifunga bao la kwanza na Yondani akipachika la pili kupitia mkwaju wa penati
Kisha ikapata ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Stand United kwenye mchezo wake wa pili, Makambo hakufunga katika mchezo huo
Mchezo wa tatu ulikuwa dhidi ya Coastal Union, Yanga ikishinda kwa bao 1-0 ambalo liliwekwa kambani na Heritier Makambo
Hivyo mpaka mechi tatu zinakamilika, Makambo alikuwa amefunga mabao mawili kama ilivyo kwa Molinga msimu huu
Wakati mjadala kuhusu ubora wa Molinga ukiendelea, mpaka sasa mshambuliaji huyo 'amefungana' na Makambo wote wakipachika mabao mawili baada ya mechi tatu
Makambo alimaliza msimu akiwa na mabao 18, huu ndio mtihani unaomkabili Molinga ambaye atahitaji kufunga mabao sio chini ya 18 ili kuwanyamazisha wakosoaji wake
Kocha Mwinyi Zahera ameonyesha kumuamini mshambuliaji huyo akimuwekea ahadi ya kufunga sio chini ya mabao 20