Leo ni siku muhimu kwa mashabiki wa soka nchini hususani mashabiki wa Yanga ambao timu yao saa 10 jioni itashuka uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Pyramids Fc kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho
Yanga, mabingwa wa kihistoria Tanzania wana dakika 180 kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho kwa mara ya tatu
Lakini pia mafanikio yao ni faida kwa Tanzania kwani wataiongezea nchi pointi huko CAF na pengine Tanzania kuendelea kuwa na timu nne kwenye michuano ya mwakani
Matokeo ya ushindi leo yanaweza kuwa hatua nzuri kuelekea makundi ingawa bado watakuwa na kazi ya kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mchezo wa marudiano ambao utapigwa wiki ijayo nchini Misri
Yanga imejifua takribani wiki nzima kujiandaa na mchezo huo, leo ndio siku ya kumaliza kazi pale CCM Kirumba
Ari na morali ya wachezaji iko juu, hali iko hivyo kwa mashabiki ambao siku ya jana mji wa Mwanza gumzo kubwa lilikuwa mchezo huo
Hakuna shaka mashabiki wengi watajitokeza CCM Kirumba kuiunga mkono timu yao, wale waliombali wataushuhudia mchezo huo kwenye runinga
Pamoja na yote yanayozungumzwa kuhusu klabu ya Pyramids Fc, hakuna lisilowezekana kwenye soka, muhimu zaidi Yanga itakuwa nyumbani
Faida ya uwanja wa nyumbani pamoja na uzoefu wa michuano hiyo ni silaha muhimu kwa Yanga leo
Pamoja na utajiri wao, Pyramids Fc ni timu changa, hii ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano ya vilabu barani Afrika
Wanaweza kuwa timu bora lakini kama Yanga itautumia vyema ugeni wao, hakuna sababu ya kukosa ushindi leo
Kila la kheri Yanga, kila la kheri wawakilishi wa nchi..