Hesabu ya Yanga leo ni kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi kombe la Shirikisho
Waarabu wanafahamika, wanapocheza kwao si rahisi sana kuwafunga lakini hawatishi wanapokuwa ugenini
Hivyo kocha Mwinyi Zahera ana kazi ya kuweka kikosi ambacho kitaweza kuipa ushindi Yanga leo
Katika mchezo huo Zahera atawakosa nyota kadhaa kama Paulo Godfrey, Maybin Kalengo, Mohammed Issa, Issa Bigirimana na Raphael Daudi, hawa wamethibitishwa kuwa hawatacheza wakiungana na Lamine Moro, Mustafa Suleyman na David Molinga ambao wana kesi tofauti
Ni wazi safu ya ulinzi itaundwa na kikosi kilichocheza mchezo dhidi ya Mbao Fc wiki iliyopita
Ali Ali anatarajiwa kuchuku nafasi ya Moro anayetumikia adhabu ya kadi mbili za njano
Upande wa kiungo pengine Abdulaziz Makame atarejea kikosini kushirikiana na Feisal Salum 'Fei Toto' wakati Tshishimbi anaweza kupewa majukumu ya ushambuliaji zaidi pengine atachukua nafasi ya Molinga ili kumsaidi Sadney Urikhob au Juma Balinya pale mbele
Hakuna shaka Mapinduzi Balama ataongoza mashambulizi akitokea pembeni kama ilivyo kwa Patrick Sibomana au Mrisho Ngasa
Upande wa kulia ambao anacheza Juma Abdul huenda ukawa 'busy' zaidi leo kwani mashambulizi mengi yanatarajiwa kupitia kwa mkongwe huyu ambaye amekuwa akipiga krosi nyingi za faida
Muhimu ni kwamba wachezaji wote wa Yanga wako tayari kwa mchezo, hakuna shaka yeyote atayepewa nafasi ya kuanza hatawaangusha Wananchi ambao leo wana kiu ya kuiona timu yao ikiibuka na ushindi