Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Amissi Tambwe amesema mabadiliko yaliyofanywa na uongozi wa timu hiyo kwa kuvunja benchi lote la ufundi, ni uamuzi uliofanywa kwa wakati sahihi
Tambwe ambaye kwa sasa anaichezea Fanja Fc ya Oman, amesema ulifika wakati ambao Yanga ilipaswa kufanya mabadiliko hayo ili kuweza kusonga mbele
Hata hivyo ametahadharisha viongozi wanapaswa kuwa makini katika kutafuta mbadala wa Zahera
Tambwe amesema amekiangalia kikosi kipya cha Yanga, kina wachezaji wazuri lakini anaamini pengine mbinu za kocha ndizo zilizowafanya washindwe kuwika
"Yanga haina kikosi kibovu, kuna mambo yalikuwa yanakosewa hata sisi wengine ni vile tulikuwa na uzoefu, lakini mfumo uliokuwa unatumika msimu uliopita usingeweza kutupa mafanikio," Tambwe amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
"Sasa viongozi watulie katika kutafuta kocha sahihi asije tena kocha mwenye mbinu za kujilinda muda wote wa mchezo, ugumu mkubwa ulikuwa hapo timu lazima icheze na iwe na mbinu mbadala"
Tambwe amesema kocha anayekuja anatakiwa kuzingatia nidhamu kwa wachezaji na hivyo anapaswa kuwa mkali
"Yanga haiwezi kucheza na timu ndogo ikaomba mpira uishe, tulikuwa tunateseka sana tofauti na miaka ya nyuma, lakini kama kocha akiwa mkali kwa nidhamu na mbinu nzuri itarudi enzi zake za kutamba"
"Hatua nzuri ni kwamba maamuzi haya yamefanyika mapema wakati ligi haijaenda mbali, sasa wanachotakiwa viongozi ni kutuliza akili na kufanya maamuzi ya haraka kumpata kocha mpya"