Wakati akiendelea kukiimarisha kikosi chake baada ya kukiongoza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema tayari amebaini 'gonjwa' linalowatesa wachezaji wa timu hiyo, hivyo anafanya kazi kubwa ya kuwarejesha
Baada ya Ijumaa iliyopita kuibuka na ushindi huo katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, Mkwasa ameendelea kukijenga kikosi chake kufuatia juzi kucheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya Mkuti Market FC ya Masasi ikiwa ni siku moja baada ya kuvaana na Komabini ya Nanyumbu.
Katika mechi dhidi ya Mkuti Market FC iliyopigwa Uwanja wa Boma, Masasi mkoani Mtwara, Yanga ilikubali kipigo cha bao 1-0, ikikumbana na dhahama hiyo baada ya kuichapa Komabini ya Nanyumbu mabao 5-0 katika mchezo wake wa kwanza uliopigwa dimba la Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Hata hivyo, Mkwasa amesema tatizo kubwa alilolibaini katika kikosi cha Yanga ni wachezaji wengi kukata tamaa, jambo ambalo anatumia muda mwingi kuwajengea matumaini mapya ili kuwarejesha mchezoni.
"Tatizo kubwa ni wachezaji wengi kukata tamaa, hivyo ninachofanya kwa sasa ni kuwajenga kwa kuwarudishia matumaini ili kuweza kufanya vizuri uwanjani," alisema kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars
Mkwasa ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, alipoulizwa kuhusu malengo yake ya muda mrefu, alisema anachokisaka kwa sasa ni matokeo ya uwanjani kwa kuwa yeye ni kocha wa muda mfupi.
"Mimi sijapewa mipango ya muda mrefu, kwa sababu ni kocha wa muda, hapa ninachokitaka kwanza ni matokeo ya uwanjani na kuitengeneza timu ili kocha ajaye aweze kuendelea hapa nilipoishia ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango yake ya muda mrefu"
Jumatano iliyopita, Yanga ilitangaza kuachana rasmi na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera pamoja na kulivunja benchi zima la ufundi huku ikimtangaza Mkwasa kukaimu nafasi hiyo kwa muda wakati ikiendelea na mchakato wa kumsaka kocha mpya.
Zahera alitimuliwa ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kutolewa na Pyramids FC ya Misri kwa jumla ya mabao 5-1 kwenye mechi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, akitangaza uamuzi wa kuachana na Zahera na kuvunja benchi zima la ufundi, alisema ni baada ya kuona timu inakwenda vibaya, jambo ambalo walikaa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo na kufikia uamuzi huo