Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga leo Jumamosi, Disemba 21 2019 saa kumi kamili jioni, watashuka kwenye uwanja wa Uhuru kumenyana na Iringa United kwenye mchezo wa kombe la FA (ASFC) mzunguuko wa tatu
Yanga inaanza rasmi kampeni ya michuano hiyo kwa msimu huu ambayo msimu uliopita walitolewa hatua ya nusu fainali
Ni mchezo ambao kama utawekwa kwenye mzani, ushindi utaonekana kuelemea zaidi upande wa Yanga
Lakini ni lazima vijana wa kocha Charles Mkwasa wapambane kupata ushindi huo kwani wakati mwingine matokeo yasiyotarajiwa hutokea kwenye soka
Mkwasa, Kaimu kocha Mkuu wa Yanga amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na wana kila sababu ya kushinda mchezo huo
"Sisi tumejiandaa vizuri na malengo yetu ni kuibuka na ushindi. Hatuwezi kuwadharau wapinzani wetu kwani mpaka wamefika hatua hii, sio wabaya," alisema Mkwasa jana baada ya mazoezi ya mwisho ya kikosi chake yaliyofanyika uwanja wa Uhuru
Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu ya Yanga umewataka mashabiki wake wajitokeze kwa wingi kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa kumi kamili jioni
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema kuna jambo kubwa litafanyika kabla ya mchezo huo
Aidha amesema kampuni ya GSM, wasambazaji wakuu wa jezi za klabu ya Yanga, wameandaa utaratibu utakaowezesha mashabiki kununua jezi original uwanjani
Kutakuwa na magari maalum yatakayokuwa yakiuza jezi nje ya uwanja
Wanayanga wameaswa kuwapa sapoti GSM kwa kununua jezi original kwani wadhamini hao wamechukua jukumu la kuirejesha Yanga mahali pake baada ya kumwaga fedha kwenye usajili wa dirisha dogo unaoendelea pamoja na kulipa mishahara ya wachezaji
Kununua jezi original chapa ya GSM zinamfanya shabiki kuwa ameichangia Yanga na kuwa amechangia maboresho yanayofanywa na kampuni hiyo
Viingilio katika mchezo huo ni 3,000/= mazungumzo na VIP ni Tsh 5,000/=