Yanga imemrejesha Jangwani, kiungo wake fundi, Haruna Niyonzima na taarifa hizi zimempa furaha na faraja kubwa straika wa zamani wa klabu hiyo, Amissi Tambwe aliyedai anaamini Mnyarwanda huyo ana uwezo mkubwa wa kuisaidia timu hiyo katika vita ya ubingwa.
Tambwe aliyeachana na Yanga msimu huu na kutimkia zake Uarabuni alikokuwa akiichezea Fanja SC ya Oman kabla ya kuvunja mkataba kutokana na matatizo ya kifamilia, alisema Niyonzima ni kati ya wachezaji anaojivunia kucheza nao klabu moja, alijua namna ya kumtengenezea mabao.
"Niyo (Niyonzima) niliishi naye vizuri. Nadhani Yanga wamefanya maamuzi sahihi ya kumrudisha, unajua maisha ya mpira ndivyo yalivyo, kuna muda unaweza kuondokana sehemu na ukarejea tena," alisema Tambwe na kuongeza;
"Alinijulia kunichezesha, nakumbuka vile ambavyo tulikuwa tukifanya mawasiliano ya akili, kuna muda nilikuwa nikipenya nakutana na pasi zake. Bado ana uwezo wa kuendelea kucheza, kikubwa ni mashabiki wa Yanga kumpokea vizuri"
Niyonzima aliichezea Yanga kwa miaka sita kuanzia 2011 hadi 2017 na kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, alivyotua Simba hakuwa na mwanzo mzuri kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Lakini alivyokaa sawa alikuwa moto wa kuotea mbali, mkataba wake ulipomalizika, viongozi wa Simba waliamua kuachana naye ndipo alipoamua kurejea kwao Rwanda ambako alikuwa akiichezea AS Kigali.