Ni wazi sasa Yanga imeanza kusakata lile kabumbu ambalo mashabiki walikuwa wakilisubiri kwa hamu
Kwa takribani misimu mitatu, Yanga haikuwa na ubora ambao umeanza kuonekana sasa pamoja na kuwa ilifanya vizuri kwenye mechi nyingi
Tangu mchezo dhidi ya Azam Fc, Yanga imeonyesha utofauti, wachezaji wako huru kuonyesha vipaji vyao na kwa kweli wameanza kuuwasha moto
Kocha Luc Eymael anapendelea soka la kupendeza 'sexy football' na anataka timu yake ipate ushindi huku ikicheza kandanda hilo la kuvutia
Lakini pia, ujio wa nyota wapya dirisha dogo wakiongozwa na Haruna Niyonzima na Bernard Morrison umechangia kuinua viwango vya wachezaji wengine
Kwa jinsi Yanga inavyocheza sasa, utabaini kikosi kimesheheni wachezaji wengi wenye vipaji, mfumo uliokuwa unatumika hapo awali ulikuwa ukiwanyima uhuru wa kuonyesha vipaji vyao
Mapinduzi Balama anayecheza kikosi cha Eymael ni tofauti na yule aliyekuwa akicheza kikosi cha Zahera
Amekuwa bora zaidi na ametengeneza pacha maridadi sana na Niyonzima
Jaffar Mohammed alikuwa akitumika kama beki wa kushoto kwa dharura tu, lakini sasa anaonekana kumudu vyema nafasi hiyo huku akionyesha uwezo mkubwa
Pengine atampa wakati mgumu Adeyum Saleh ambaye usajili wake ulikuwa maalum kwa ajili ya kuondoa changamoto ya nafasi hiyo
Leo Said Juma Makapu amepewa nafasi na kuonyesha uwezo mkubwa kwenye safu ya ulinzi
Ni mchezaji ambaye alikuwa hapewi nafasi kabisa wakati wa Zahera lakini tangu ameanza kucheza sambamba na Moro, Yanga imeruhusu bao moja tu katika michezo miwili iliyopita
Kwa Makapu wa sasa, mkongwe Kelvin Yondani, Ally Mtoni na Andrew Vicent 'Dante' inabidi wakae sawa
Kwa kiasi kikubwa Eymael amefanikiwa kurejesha morali ya wachezaji na sasa wana-enjoy soka kama asemavyo Mrisho Ngasa
Kwa ubora wa wachezaji wa Yanga, leo hii Eymael anaweza kutumia timu tofauti kwenye kila mchezo na akapata matokeo
Shikhalo, Boxer, Adeyum, Dante/Sonso, Yondani, Feisal, Ngasa, Banka, Nchimbi, Tariq, Sibomana hiki ni kikosi kingine kabisa ambacho kinaweza kushinda mchezo wowote ukiachana na kikosi kilichoichapa Prisons 2-0 jana