Mchezo wa ligi kuu ya Vodacom kati ya Yanga dhidi ya Mbeya City umemalizika kwa timu hizo kugawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1
Mbeya City walitangulia kufunga bao la kuongoza, beki Lamine Moro akiwazawadia bao hilo baada ya kujifunga akiwa kwenye jitihada za kuondosha hatari langoni
Kukosekana kwa mawasiliano kati yake na mlinda lango Metacha kulipelekea kuwazawadia Mbeya City bao hilo
Yanga ilikuwa bora zaidi kipindi cha pili hasa baada ya mkufunzi wa timu hiyo Luc Eymael kumuingiza nahodha Papy Tshishimbi nafasi ya Said Juma Makapu ambaye hakuwa na mchezo mzuri sana kwenye kipindi cha kwanza
Tshishimbi alisaidia kuipeleka timu mbele huku wakati mwingine mwenyewe akipanda kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji
Baada ya kosakosa nyingi, Yanga ilisawazisha bao hilo kwenye dakika ya 78 mfungaji akiwa Bernard Morrison
Mchezo huo ulisimama mara kwa mara kutokana na wachezaji wa Mbeya City kutumia mbinu ya kupoteza muda
Hadi dakika 90 zinakamilika, mchezo uliisha kwa sare ya bao 1-1
Sio matokeo ambayo mashabiki wa Yanga wameyafurahia sana hasa ikizingatiwa leo timu hiyo inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 85, tangu kuundwa kwake
Matokeo ya ushindi yangenogesha zaidi siku hii muhimu kwa Yanga