Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima amesema ni vyema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likaweka subira katika kuchukua uamuzi kuhusu hatma ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu
Katika siku za karibuni kumeshuhudiwa nchi mbalimbali duniani zikichukua hatua ya kumaliza misimu yao pasi na kuchezwa mechi zilizobaki kutokana na changamoto iliyosababishwa na ugonjwa wa corona
Akizungumza jijini Dar es salaam jana, Niyonzima alisema anaamini Tanzania bado ina mwezi mmoja wa kusubiri kabla ya kuchukua maamuzi
"Kwa maoni yangu, ningependa tucheze mechi zilizobaki ili kila timu ipate haki yake uwanjani. Japo hatujui janga la corona litamalizika lini, ila ningependa tucheza kwa sababu bado tuna mwezi mmoja. Ligi inatakiwa kumalizika mwezi huu ila kama itatokea tofauti naamini wataangalia uamuzi sahihi wa kuchukua"
"Lakini mimi ningependa TFF wavute subira maana tunaweza kucheza na upande wetu Yanga tunaweza kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kama hatutaweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu," amesema
Juzi kocha mkuu wa Yanga Luc Eymael alitoa mapendekezo kama hayo kwa TFF akitaka uwekwe utaratibu wa kuwezesha mechi zilizobaki kuchezwa bila ya mashabiki
Eymael alishauri mechi zote kuchezwa kwenye vituo maalum ambapo wachezaji, makocha na viongozi watafanyiwa vipimo kabla ya mechi kuruhusiwa