Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Saidi amesema kiungo wa Simba Said Khamis Ndemla sio miongoni mwa wachezaji ambao watasajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao
Ndemla amekuwa akihusishwa kutaka kusajiliwa na Yanga, uvumi ambao umekuwa ukijitokeza kila dirisha la usajili
Hersi ambaye anatembea na faili lenye orodha ya wachezaji wanaotarajiwa kusajiliwa na Yanga, amesema timu hiyo itafanya usajili wa maana ambapo nyota wote wakaowasajili sio wa kuja kukaa benchi
"Hilo suala la Ndemla ni tetesi tu wala hayupo kwenye mipango yetu. Namuheshimu ni mchezaji mzuri, lakini nikuhakikishie sio miongoni mwa wachezaji tunaowataka. Sidhani kama kuna mchezaji yeyote tutamsajili kutoka klabu ya Simba," alisema Hersi
Kuhusu usajili watakaofanya, Hersi amesema wachezaji wapya watakaosajiliwa na Yanga wanafuatiliwa kwa umakini na wataalam washauri waliopewa jukumu la kuwafanyia tathmini
"Wachezaji tutakaowaleta sio wa kukaa benchi. Kwanza huko kwenye vilabu vyao kigezo cha kwanza ni lazima wawe wanacheza. Tumewapa kazi wataalam ambao watawafanyia tathmini kisha kutupa maoni yao"
Hersi amesema wamejipanga kuunda kikosi kitakachokuwa na uhakika wa kutwaa ubingwa msimu ujao