Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amewataka Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo wasiyumbishwe wakati huu ambao timu inaelekea kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo
Mwakalebela amebainisha kuwa uongozi chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla, umejipanga kukamilisha mchakato huo huku akiwapa shukrani GSM ambao wamejitolea kugharamia mchakato wote
Amesema Kamati ndogo ya Mabadiliko inayoongozwa na Wakili Alex Mgongolwa imefanya kazi kubwa na amewahakikishia Wanayanga kuwa muundo watakaoufuata utaibakisha klabu mikononi mwao
Mwakalebela amesema wadau wamepewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu mchakato huo hivyo kwa wakati huu Wanayanga wanapaswa kuwapuuza wote ambao watajaribu kupinga mchakato huo kwani wanapaswa kuwasilisha maoni yao klabuni
"Tunafahamu kuna watu wanapinga, lakini hawana hoja kwani tumewakaribisha kwa maoni hawaji, hivyo katika hili tunaangalia maslahi ya Klabu na ya walio wengi, ndio maana tunawaomba wanachama watuunge mkono kwani watatoa maoni yao, na watafanya maamuzi kwa msingi wa kidemokrasia kama ilivyo kawaida ya klabu yetu," Mwakalebela aliiambia tovuti ya Yanga
Aidha, ameongeza kuwa Mkataba na La Liga utasainiwa wakati wowote baada ya kampeni na hamasa inayoendelea kumalizika
Mchakato wa Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Yanga utafanyika kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza itaanza punde tu baada ya kusainiwa mkataba na La Liga, awamu hiyo itachukua miezi sita
Inaelezwa La Liga watashiriki moja kwa moja katika awamu ya kwanza ili kuweka misingi ya mfumo huo mpya
Awamu ya pili na ya tatu zitaendelea chini ya uongozi wa Yanga ambapo mchakato mzima umepangwa uwe umekamilika katika kipindi cha miezi 30