Nahodha Msaidizi wa Yanga Juma Abdul amewashukuru mashabiki wa timu hiyo mkoani Shinyanga kwa kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mwadui Fc
Mchezo huo uliopigwa jana kwenye uwanja wa CCM Kambarage, uliwashuhudia mabingwa hao wa kihistoria wakipiga shoo ya kibabe na kuondoka na ushindi wa bao 1-0
"Tunawashukuru mashabiki wetu kwa kuja kwa wingi kutuunga mkono. Tulifahamu mchezo huu tunahitaji kushinda hasa baada ya matokeo tuliyopata kwenye mchezo wa kirafiki wiki iliyopita," alisema Abdul
"Tulihitaji kuwapa futaha mashabiki na kuwahakikishia kuwa bado tuko imara.Β Tulikuja hapa Shinyanga na lengo la kuondoka na alama zote tatu, tunashukuru tumefanikiwa"
Aidha Abdul alizungumzia sintofahamu iliyojitokeza kwa baadhi ya wachezaji kufanya mgomo kuelekea mchezo huo, ambapo amesema baada ya kocha Luc Eymael kuwasili mkoani Shinyanga walimaliza tofauti zao
"Kabla ya mchezo, benchi la ufundi, sisi wachezaji na viongozi tulifanya kikao na kumaliza sintofahamu iliyokuwepo na ndio maana leo umeona tumeingia uwanjani tukiwa wamoja"
Katika kikao hicho kilichofanyika juzi, mshambuliaji David Molinga aliwaomba radhi wachezaji wenzake kwa kitendo ya kutoongozana na timu
Ujio wa nyota huyo mkoani Shinyanga ulitaka kuchafua hali ya hewa baada ya baadhi ya wachezaji akiwemo beki kisiki Lamine Moro kugoma kufanya nae kazi
Kocha Eymael hakumtumia Molinga kwenye mchezo wa jana pamoja na kuwa alikuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba