Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael leo huenda akamrejesha kikosini kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali, utapigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma kuanzia saa kumi jioni
Fei Toto hakuwa sehemu ya kikosi kilichoikabili Mwadui Fc mwishoni mwa wiki na kupata ushindi wa bao 1-0 mkoani Shinyanga
Kiungo huyo fundi alikuwa akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano huku ikilelezwa pia alipata majeraha madogo
Kwenye mchezo dhidi ya Mwadui Fc, Eymael alimtumia mkongwe Kelvin Yondani nafasi ya kiungo mkabaji
Eymael alieleza kufurahishwa na uwezo ulioonyeshwa na nyota huyo ambaye amezoeleka kucheza nafasi ya ulinzi wa kati
Lakini kutokana na majeraha ya Lamine Moro ambaye huenda asiwe sehemu ya kikosi leo, Yondani anaweza kurudishwa katika nafasi ya ulinzi na Fei Toto kucheza sehemu ya kiungo sambamba na Haruna Noyonzima
Lakini pia Eymael leo anaweza kumrejesha kikosini kinara wa mabao David Molinga ambaye mchezo uliopita alipewa dakika chache
Winga Deus Kaseke, mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri kwenye mchezo uliopita, nae anaweza kulinda nafasi yake kwa mchezo wa pili mfululizo