Afisa Mhamasishaji wa klabu ya Yanga Antonio Nugaz amewataka mashabiki wa klabu hiyo wawe na amani kwani timu yao haiwezi kufungwa na Simba kwenye mchezo wa nusu fainali kombe la FA ambao utapigwa Julai 12 katika uwanja wa Taifa
Baada ya Simba kutinga nusu fainali kwa kuichapa Azam Fc mabao 2-0 katika mchezo ambao waliutawala, mashabiki wa timu hiyo wametamba kuwa Yanga hawatatoka Julai 12
Nugaz amesema wao wamefurahi kukutana na Simba katika hatua hiyo kwani wana uhakika hawawezi kuwasumbua
"Siku zote watani wanapokutana mechi zao zinakuwa na utani mwingi, lakini ukiangalia matokeo ya nyuma sisi ni zaidi yao. Tunaamini utakuwa mchezo mzuri wenye ushindani kwa sababu sisi tuliwapasua kwenye mchezo uliopita, nao watataka kulipa kisasi"
"Lakini bila ya makandokando tuucheze mpira halafu matokeo yapatikane baada ya dakika 90, sisi hatufungwi. Nawaambia mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi HATUFUNGWI," alitamba Nugaz