Nadhani kuna haja kwa uongozi wa Yanga kuachana na mshambuliaji Bernard Morrison ambaye ameendelea kuikosea heshima Yanga pamoja na wadhamini wao GSM ambao ndio waliofanya jitihada kumleta chini baada ya mapendekezo ya kocha Luc Eymael
Tukio alilofanya baada ya kutolewa jana, sio kwamba linaikosea heshima Yanga tu bali hata TFF kama wasimamizi wa soka nchini.
Halikuwa tukio la kiungwana kumsukuma msimamizi wa mchezo ambaye alifanya jitihada za kumzuia asivunje taratibu kwa kutoka nje baada ya kufanyiwa mabadiliko
Hivi huyu Morrison anadhani yeye ni nani ndani ya klabu ya Yanga? Sidhani kama anastahili kuvaa tena uzi wa Yanga
Kama ana mkataba wa muda mrefu na hataki kuutumikia basi sheria ifuate mkondo wake, alipe gharama za mkataba kisha aachwe ajiunge na timu yoyote anayotaka hata kama ni Simba
Kwani kuendelea kukaa nae klabuni bila kumtumia pia itakuwa hasara kwa klabu kwani italazimika kumlipa mshahara
Wachezaji wenzake walionesha kuchukizwa na kitendo alichofanya achilia mbali tuhuma za kufanya hujuma kwa kucheza chini ya kiwango kwenye mchezo huo