Tetesi zimekuwa nyingi juu ya 'panga' linalotarajiwa kupitishwa na mabosi wa Yanga katika dirisha la usajili ambalo litafunguliwa wiki ijayo baada ya msimu wa ligi kuu kufikia tamati siku ya jumapili
Lakini unaweza kushangaa kusikia jina la Mrisho Ngasa nalo limekuwa likitajwa sana na baadhi ya magazeti na vyombo vya habari kuwa anaweza kuwa miongoni mwa watakaopewa mkono wa kwaheri
Ukizungumzia wachezaji Yanga 'lialia' huyu Ngasa ni mmoja wao. Uyanga wake anauonyesha kwa vitendo anapokuwa uwanjani, anajituma na mchango wake huonekana waziwazi
Huyu anastahili kuendelea kubaki sio tu kwa sababu ana mapenzi makubwa na Yanga, lakini hata uwezo wa kuitumikia Yanga bado anao
Tangu kurejea kwa ligi baada ya mapumziko ya corona, ukitaja wachezaji watatu ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Yanga, unaweza kumtaja Ngasa, Deus Kaseke na mwingine anaweza kuwa Feisal Salum 'Fei Toto'
Hawa ni wachezaji ambao ukiwaona uwanjani, unapata matumaini kuwa jambo lolote linaweza kutokea
Uongozi wa Yanga unaweza kufanya makosa kama utaamua kuachana na Ngasa. Kwani kwa wachezaji wa ndani sidhani kama wapo wengi wanaomzidi ubora licha ya umri wake wa miaka 31
Yanga imara ya msimu ujao itawahitaji wachezaji wakongwe kama Ngasa, ambao wao watawahamasisha wageni wafahamu thamani ya kuchezea klabu kubwa ya Yanga