Ukiona wachezaji wengi wanaosajiliwa na timu nyingine kuwa lazima wahusishwe na Yanga, hilo linadhihirisha ukubwa wa Yanga
Lakini pia ni wazi Yanga ndio klabu yenye kitengo bora cha kusaka wachezaji, ndio maana kila mmoja huko anasubiri kusikia Yanga wanataka kumsajili nani
Ni juzi tu wamemuongeza Senzo Mazingisa, mbobezi wa soka la Afrika
Amini, usiamini mpaka sasa Yanga haijanyan'ganywa mchezaji waliyemtaka kama walivyosisitiza viongozi wenyewe
Walishafahamu kuwa timu nyingine zinasubiri tetesi zao ili zisajili hivyo katika usajili unaoendelea, vijana wa mjini wanasema Yanga ilitegesha 'matango pori' mengi sana
Usajili waliofanya Yanga sio wa kushindana na Simba kama wanavyofanya wao, Yanga ilijiwekea malengo ya kushinda ubingwa wa ligi kuu msimu ujao na ikitokea wanapata nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa wakafanye vizuri huko
Angalia usajili uliofanyika mpaka sasa, hakuna mchezaji aliyesajiliwa kwa bahati mbaya, wote walihitajika
Tatizo letu mashabiki tunapenda ikifika wakati wa dirisha la usajili, timu itangaze usajili mpya kila siku bila ya kujali malengo yaliyowekwa
Msimu uliopita Yanga ilisajili wachezaji wengi kwa pupa lakini nini kilichotokea?, asilimia 98 ya wachezaji waliosajiliwa hawapo sasa, wameachwa, timu imepata hasara. Hivi mashabiki tumewahi kulifikiria hili?
Ilishaelezwa kuwa usajili wa nyota wa kigeni ulishakamilishwa. Kilichochelewesha wachezaji hao ni kufungwa kwa anga kwa nchi wanazotoka kutokana na janga la corona
Nchi nyingi zimefungua anga wikiendi hii hivyo inatarajiwa wachezaji hao wataanza kuwasili wakati wowote. Kaimu Katibu Mkuu Simon Patrick alitaja mpaka idadi ya wachezaji wa kigeni wanaosubiriwa, wako sita
Nadhani hapa tunapaswa kuwa na subira, tusubiri kile kilichoelezwa na viongozi, kama hakitatimia basi tutakuwa na sababu ya kuwahukumu lakini sio sasa