Beki kisiki wa Yanga Lamine Moro amerejea kwenye mazoezi ya kikosi cha timu hiyo kuelekea mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu ya Vodacom msimu wa 2020/21 dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa Jumapili kwenye uwanja wa Mkapa
Lamine alikosa mchezo wa kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Aigle Noir ambao ulipigwa Jumapili iliyopita na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
Yanga ilitumia mchezo huo kutambulisha kikosi chake cha msimu huu
Aidha, kiungo fundi Mapinduzi Balama nae ameendelea kupona majeraha yake sasa akikaribia kurejea uwanjani
Balama alipata majeraha makubwa ya kifundo cha mguu mwishoni mwa msimu uliopita
Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema Balama ndiye mchezaji pekee ambaye yuko nje ya kikosi kutokana na majeraha
Balama anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi katika kipindi cha wiki mbili
Kuelekea mchezo dhidi ya Prisons, Mwambusi amesema vijana wanaendelea vizuri na maandalizi
"Maandalizi yanaendelea vizuri, kocha (Zlatko) ameridhishwa na viwango hasa kwa wachezaji wetu wapya na matumaini yetu makubwa ni kufanya vizuri katika michezo yote ili kufikia matarajio yanayotarajiwa na wanachama na mashabiki wa Yanga," alisema Mwambusi.