Wakati uongozi wa Yanga ukisubiri kumtangaza kocha mpya, kocha msaidizi Juma Mwambusi amepewa majukumu ya kukiandaa kikosi cha timu hiyo kuelekea mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa Oktoba 18 uwanja wa Benjamin Mkapa
Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Burundi Cedric Kaze ndiye anayetarajiwa kutangazwa kuchukua nafasi ya Zlatko Krmpotic lakini kwa muda uliobaki kuelekea mchezo huo, huenda akamuacha Mwambusi aiandae timu ili kuhofia kuwachanganya wachezaji kuelekea mchezo huo mkubwa
Mwambusi ndiye aliyekiandaa kikosi cha Yanga kuelekea mchezo wa kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Aigle Noir kabla ya ujio wa Krmpotic
Wengi wanaamini mchezo ule ndio ulikuwa wa mwisho kwa Yanga kucheza soka la burudani kwani baada ya Krmpotic kutua mambo yakabadilika
Jana Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM alisema kuwa wamekubaliana kuwa Mwambusi ataendelea na majukumu ya kukinoa kikosi wakati wakikamilisha mchakato wa kocha mpya
"Tulimuondoa Zlatico kwakuwa tulikuwa hatulidhishwi na mpira wake, falisafa yake na mengine. Kwa sasa timu itakuwa chini ya Mwalimu Juma Mwambusi mpaka hapo kocha mpya atakapokuja," Hersi aliiambia eFM Radio