Serikali imejipanga kudhibiti mapato kwenye mchezo wa watani wa jadi wa Yanga na Simba unaotarajiwa kufanyika Oktoba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Serikali imedhamiria kuja na mfumo mpya baada ya kupatikana mapato madogo katika michezo ya msimu uliopita iliyowakutanisha watani hao wa jadi licha ya kuhudhuriwa na watazamaji wengi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas, alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha timu zinapata haki inayostahili kwa viingilio vitakavyopatikana kutoka kwa mashabiki watakaojitokeza.
"Kama serikali tumeanza kufanya utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwamo ukarabati wa Uwanja wa Mkapa ambao kwa sasa uko tayari kwa mechi zote kubwa na pili kwenye mchezo wa watani tumejipanga kuthibiti mapato ili timu ziweze kupata haki yao wanayostahili," Dk Abbasi alinukuliwa na gezeti la HabariLeo
Alisema moja ya mikakati waliyojiwekea kutimiza lengo hilo ni kuhakikisha mashabiki wote wanakuwa na N-kadi (kadi inayomuwezeha mtu kuingia uwanjani) ili aweze kuingia uwanjani siku ya mchezo.
"Mashabiki wanatakiwa kuwa na N-kadi itakayowawezesha kununua tiketi kupitia simu zao za mkononi na huu ni utaratibu mpya tulioanzisha ili kuwathibiti baadhi ya watu wanaoibia serikali na timu mapato," alisema.
Alisema ili kutatua changamoto ya viwanja, serikali inaendelea na utekelezaji kwenye maeneo mbalimbali, ikiwamo kufanya ukarabati na kuandika jina la Benjamini Mkapa kwenye uwanja huo ambao hapo awali ulikuwa ukiitwa Uwanja wa Taifa.
"Sasa ni rasmi unaitwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na wadau tunawajibu wa kuendelea kumuenzi Mzee Mkapa," alisema.
Dk Abbas amewataka mashabiki waheshimu uwanja huo na waache tabia ya kuvunja viti na kwamba mchakato wa kujenga uwanja mkubwa zaidi ya wa Mkapa unaendelea Dodoma ambao michoro imeshakamilika.
Aidha, alisema serikali imejipanga kuiunga mkono timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kuelekea kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi.
"Serikali tunawatakia kila la kheri wafanye vyema wasituangushe, tupo nyuma yao tunajua mchezo una umuhimu kwa vijana wetu kujiandaa na mashindano makubwa mbeleni," alisema Dk Abbas.