Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Amissi Tambwe ameupongeza uongozi wa mabingwa hao wa kihistoria kwa kumuajiri Cedric Kaze kuwa kocha mkuu wa timu hiyo
Tambwe aliyewahi kuitumikia Vital'o ya Burundi wakati Kaze akiinoa klabu ya Atletico ya nchini humo, amesema anamfahamu kocha huyo, anafundisha soka la chinichini
Aidha Tambwe amesema ni muhimu kwa Wanayanga kutompa presha kocha huyo ili aweze kuunda timu imara ambayo ana uhakika itafanya vizuri

"Kaze ni kocha mzuri kutokana na jinsi ninavyomjua tangu zamani wakati nacheza VitalβO hapa Bujumbura, yeye alikuwa akifundisha Atletico, kweli timu yake ilikuwa inacheza mpira wa chini wenye pasi nyingi," alisema Tambwe
"Nadhani labda kitu ambacho kinaweza kusumbua ni hizo presha za hapo Tanzania, Lakini nje ya hapo Kaze ni kocha mzuri, anafundisha mpira wa chini siyo wa kutupa tupa yaani ule wa kubutua butua naamini atawasaidia sana Yanga kwa kuifanya icheze mpira mzuri, wapinzani wanatakiwa kujiweka sawa kweli"
Kaze aliondoka Burundi mwaka 2012 kuelekea kule nchini Ujerumani ambapo alipata mafunzo ya juu ya ukocha na akapata nafasi ya kufanya kazi na timu ya Taifa ya Ujerumani
Baadae akapata fursa ya kuwa mkufunzi katika Academy za Fc Barcelona, akifanya kazi hiyo Ujerumani na Canada
Amewahi kuinoa timu ya Taifa ya Burundi ambapo mwaka 2012 alichaguliwa kuwa kocha bora wa CECAFA
Wanayanga wanasubiri ujio wake, taarifa zimebainisha kuwa Kaze anatarajiwa kuondoka nchini Canada kesho Jumatatu au Jumanne na huenda akawasili nchini siku ya Alhamisi