Paulo Godfrey 'Boxer' ni miongoni mwa vipaji ambavyo Wanayanga walikuwa na matumaini makubwa kwake baada ya kuwa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha Yanga
Msimu wa 2018/19 ndio uliomtambulisha Boxer baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga wakati huo Mwinyi Zahera kumpandisha kwenye kikosi cha kwanza kutoka Yanga B
Msimu uliopita haukuwa mzuri kwake kutokana na changamoto nyingi za majeruhi zilizomfanya akae nje kwa muda mrefu
Msimu huu hakufanikiwa kuingia kabisa kwenye kikosi cha Zlatko Krmpotic lakini ujio wa kocha Cedric Kaze unaweza kuwa na neema kwake
Kaze ni kocha wa kipekee kwani alijipa muda wa kuwasoma wachezaji wake, akifuatilia viwango vyao katika misimu miwili ya karibuni
Boxer ni miongoni mwa wachezaji ambao alikuwa na mawasiliano nae kabla hajatua nchini
Boxer amefichua kuwa Kaze alimpigia simu kabla hajatua nchini akimuulizia kwa nini hamuoni uwanjani wakati anatambua ni mchezaji mwenye kipaji
"Ni kweli kocha niliwasiliana nae, akaniuliza maendeleo yangu, nikamwambia nilikuwa na majeruhi lakini sasa naendelea vizuri," alisema Boxer
Hata alipotua kule Avic Town, Boxer ni miongoni mwa wachezaji ambao walifanya mazungumzo binafsi na Kaze
Bila shaka msimu huu Wanayanga watarajie mambo mazuri kutoka kwa Boxer kwani ni wazi chini ya Kaze kama hatasumbuliwa na changamoto ya majeraha, tunaweza kumuona Boxer yule wa wakati wa Zahera