Mara ya mwisho mchezo wa ligi kuu kati ya Yanga dhidi ya Polisi Tanzania uliopigwa uwanja wa Uhuru, ulishuhudia timu hizo zikitoka sare ya mabao 3-3
Ni mchezo ambao Wanayanga kwa upande mmoja hawawezi kumsahau Ditram Nchimbi 'Duma' ambaye alifunga mabao yote matatu ya Polisi Tanzania. Shukrani kwa mabao mawili ya David Molinga ambayo yaliinusuru Yanga kupoteza mechi ya pili mfululizo ligi kuu ya Vodacom msimu uliopita
Lakini mchezo huu ndio uliofungua ukurasa mpya kwa Nchimbi kwani ulikuwa mwanzo wa yeye kutambulika, aliitwa timu ya Taifa na baadae akasajiliwa na Yanga
Leo Nchimbi anarejea tena uwanja wa Uhuru lakini sasa akiwa upande wa pili, Yanga
Kama kocha Cedric Kaze atampa nafasi ya kucheza, atahitaji kufanya kile alichokifanya mwaka jana au afanye zaidi ili aendelee kutunza historia nzuri aliyoiweka katika uwanja huo
Kwake utakuwa ni mchezo ambao atahamasika sana kuhakikisha anafanya kitu, ili ikawe zawadi kwa mashabiki wa Yanga ambao msimu uliopita aliwapa machungu